Monday, February 27, 2012
Watanzania wachemka Kili Marathon
Wanariadha wa Kenya, Ezekiel Kimath (kushoto) Kimot Chemo na David Kipromo, wakiongoza mbio za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika mjini Moshi jana. Wanariadha hao walitamba kwa kuchukua nafasi zote 20 za juu kwa upande wa wanaume na wanawake. Picha na Mussa Zumba.
TANZANIA imeendelea kuwa msindikizaji katika medani ya kimataifa baada ya wanariadha wake pekee, Fabian Joseph kushika nafasi ya tatu kwa upande wa wanaume na Mary Naali kushika nafasi ya tano kwa upande wa wanawake katika mbio za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Wakati hali ikiwa mbaya kwa wanariadha wa Tanzania, Kenya imeendelea kutawala mbio hizo baada ya wanariadha wake (wanaume kwa wanawake) kukamata nafasi zote tatu muhimu za juu katika mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Premium Lager na Nusu Marathon Kilometa 21.
Katika mbio hizo, Joseph alikamata nafasi ya tatu katika mbio za nusu marathon kwa upande wa wanaume baada ya kutumia saa 1:03:32 na kuzawadiwa medali ya shaba wakati Naali alikamata nafasi ya tano katika mbio za nusu marathon baada ya kutumia saa 1:15:47 kwa upande wa wanawake.
Umahiri wa Wakenya ulianzia katika mbio za Kilimanjaro Marathon za Kilometa 42 kwa upande wa wanaume, ambapo David Kipron aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 2:13:57, wakati Ezekil Kimtai alikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 2:14:06 huku Kibeth Timoth akimaliza mshindi wa tatu kwa kutumia saa 2:15:38.
Uhodari huo wa Wakenya hao uliendelea kwa upande wa wanawake ambapo Monica Jopkoech alimaliza mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 2:42:45 wakati Peris Jepkorir alishika nafasi ya pili baada ya kutumia saa 2:43:02 na Panuelag Anesomi alitwaa nafasi ya tatu akitumia saa 2:43:41.
Katika mbio za nusu marathon, Hosea Mallel aliendeleza wimbi la ushindi kwa Wakenya alipotumia saa 1:03:00 na kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume, wakati Ngengi Jofrey alikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 1:03:32 na kumwacha Mtanzania Joseph akikamata nafasi ya tatu alipotumia saa 1:03:14.
Naye Vicoty Chepkemoi alikuwa mbabe kwa upande wa wanawake alipoibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 1:13:00, huku Wakenya wenzake Cythia Limo akikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 1:13:07 na Flomena Daniel aliyemaliza akiwa katika nafasi ya tatu baada ya kutumia saa 1:14:48.
Kivumbi kingine kilikuwa katika mbio za kujifurahisha, ambapo Gareth Ismail aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume wakati Brazil Boy alishika nafasi ya pili na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Fabia Nelson wakati ambapo Jaquline Juma aliibuka mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanawake, akimwacha Catherine Yuko katika nafasi ya pili na Nathaniel Elisante aliyemaliza katika nafasi ya tatu.
Washindi wa kwanza wa mbio za Kilimanjaro Marathon (wanawake na wanaume) walizawadiwa Sh 6 milioni, Sh 3 kwa washindi wa pili na 1,500,000 kwa washindi wa tatu,huku zawadi hizo zikiendelea katika mtitiriko wake.
Naye mshindi wa pili wa mbio za nusu marathon (wanaume kwa wanawake) walizawadiwa Sh 3 milioni, mshindi wa pili Sh 1,500,000 na mshindi wa tatu Sh 750,000 kwa mtiririko wake huku washindi wa mbio nyingine kama za kujifurahisha na Gapco pia walipata zawadi mbalimbali ikiwamo fedha taslimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment