HOSPITALI ya Mkoa wa Arusha Mount Meru imeingia kwenye kashfa baada ya baadhi ya madaktari wake na wauguzi kutuhumiwa kusababisha kifo cha mjamzito ,Florence Joseph (34) mkazi wa Sokoni one jijini Arusha.
Mwili wa marehemu huyo pamoja na kichanga chake tayari imezikwa juzi katika makaburi ya Njiro yaliyopo nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo,Dk Omar Chande alipohojiwa kuhusu tukio hilo alisema kwamba bado hajapokea taarifa hiyo, lakini aliahidi kufuatilia kwa kina kabla ya kutoa ufafanuzi wa kina.
Akisimulia kisa hicho jirani wa wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Katrina Kimaro katika eneo la msiba huo alisema kwamba Febuari 19, mwaka huu saa 10.00 jioni alimsindikiza marehemu kujifungua katika Hospitali ya Levolosi iliyopo jijini hapa baada ya kushikwa na uchungu mkali.
Alisema kwamba mara baada ya kufika hospitalini hapo madaktari katika hospitali hiyo walimpima na kisha kushauri apelekwe haraka Hospitali ya Mount Meru kutokana na kuona njia ya kujifungua ikiwa ndogo.
Katrina, alisema kwamba walifika katika hospitali hiyo saa 12.00 jioni ambapo moja kwa moja waliwasili eneo la mapokezi na kuambiwa wasubiri watahudumiwa lakini cha ajabu kila daktari aliyekuwa akipita eneo hilo alikuwa akiwashangaa.
Alisema kwamba wakati wanaendelea kusubiri katika eneo la mapokezi hospitalini hapo marehemu alikuwa akilalamika mara kwa mara kwamba anasikia uchungu mkali ndipo alipowafuata wauguzi waliokuwapo katika chumba cha mapokezi lakini walimjibu wana shughuli nyingi zinazowaingizia pesa.
“Tulipokuwa eneo la mapokezi marehemu alikuwa akijisikia uchungu mkali kila mara analalamika ikabidi mimi niwafuate wauguzi niwaeleze lakini cha ajabu walinijibu kwamba wana kazi zingine, wanakula vichwa” alisema Kimaro.
Aliendelea kusimulia kisa hicho kwamba ilipofika saa 2.00 usiku alijitokeza daktari mmojawapo aliyewauliza shida yao na ndipo walipomweleza ambapo alifanya taratibu za marehemu kufikishwa katika chumba cha kuzalia na wao waliambiwa warudi nyumbani marehemu atahudumiwa.
Alisema kwamba kesho yake Febuari 20, alfajiri saa 11.00 alifika hospitalini hapo kujua hali ya marehemu endapo ameshajifungua au la na ndipo alipoenda moja kwa moja katika wodi ya wazazi hospitalini hapo na kumtafuta bila mafanikio.
Alisema baada ya hali hiyo ndipo alipokwenda katika ofisi za chumba cha kuzalia na kumkuta muuguzi mmojawapo na kumwulizia marehemu, lakini cha ajabu muuguzi huyo alitokomea bila kumpa jibu lolote na ndipo alipoamua kwenda katika lango kuu la hospitali hiyo kumwuliza askari aliyekuwa akilinda langoni hapo.
Kimaro, alibainisha kwamba askari huyo alimchukua na kisha kumfikisha kwa muuguzi mwingine waliyemkuta katika wodi ya wazazi akifanya usafi ambapo baada ya kumwelezea shida yake cha ajabu aliwajibu kwamba ametingwa na hawezi kuacha kufanya usafi ashughulikie suala lao.
Alidai baada ya hali hiyo ndipo alipojitokeza daktari mmojawapo baada ya kumwona akihangaika na alipomweleza shida yake akampeleka kwa muuguzi mmojawapo ambaye yuko katika ofisi za chumba cha kuzalia na alipomweleza shida yake alimjibu kwamba wanasikitika mgonjwa wake alifariki jana katika mazingira ya kutatanisha.
Kimaro alisema kwamba muuguzi huyo alimpa maelezo kwamba ilipofika saa 6.00 usiku jopo la madaktari walienda kumchunguza marehemu endapo njia ya kujifungulia imefunguka na ndipo walipompa muda saa moja na kisha kurudi tena saa 7.00 usiku ambapo walimchukua kwa lengo la kwenda kumfanyia upasuaji lakini tayari alikuwa ameshafariki dunia.
“Nakumbuka yule muuguzi alinieleza kwamba ilipofika saa sita usiku walishuka katika chumba cha kuzalia lakini wakamkuta marehemu ana uchungu mkali na njia haijafunguka ndipo walipompa saa moja tena wakarudi saa saba na kuamua kumchukua kumpeleka kumfanyia upasuaji lakini tayari walimkuta marehemu alikuwa ameshakata roho”alisema kwa uchungu
Naye, mume wa marehemu huyo ,Rashid Aloyce alilalamikia kifo cha marehemu mke wake na mtoto kwamba kimetokana na uzembe wa madaktari hospitalini hapo kwa kuwa walimwacha kwa muda wa saa saba bila kumpatia huduma yoyote pamoja na kushikwa uchungu mkali.
No comments:
Post a Comment