Pages

Tarumbeta Banner

Monday, February 27, 2012

Mayai ‘feki’ yatua Dar

AFYA za Watanzania zipo hatarini kutomkana na kuingizwa nchini kwa mayai feki, Mwananchi Jumapili limebaini. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na wafanyabiashara nchini, umebaini kuwa soko la Dar es Salaam limevamiwa na mayayi hayo yaliyoingizwa nchini kutoka Kenya na yanauzwa kwa bei rahisi huku ubora wake ukitiliwa mashaka.

Kwa mujibu wa maelezo ya wafanyab iashara hao, mayai hayo huuzwa Sh4,000 kwa trei na yanaonekana sio makubwa kama yanayopatikana nchini na yanapovunjwa hayana kiini na baadhi maji yake yamechanganyika na vitu mithili ya nyuzi zenye rangi nyekundu.

Wafanyabiashara hao wanalalamika kuwa kuingizwa nchini kwa mayai hayo yamevuruga soko la ndani ambalo trei moja ilikuwa inauzwa kwa Sh7,000 lakini hayo yanauzwa Sh4,000.

Mayai hayo yanapatikana kwa wingi maeneo ya Kariakoo na Gongo la Mboto na yanauzwa kwa wingi kwa wafanyabiashara wa vyakula jijini Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Muda wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Mayai Tanzania, Placidia Bambanza alisema mayai hayo yalianza kuingia nchini tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

“Tumepanga kupeleka malalamiko yetu kesho (jumatatu) kwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na tayari tumeandaa baadhi ya mayai hayo tumuonyeshe na atambue ubovu wake,” alisema Bambanza.

Alisema kuwa hali hiyo imewafanya nao waanze kuuza mayai kwa Sh5000 badala ya Sh7000, jambo ambalo alisema kuwa linawafanya wapate hasara kubwa.
“Tuligundua kuwa mayai haya yanatoka Kenya kwa kuwa wateja wetu ambao awali tulikuwa tukiwauzia mayai, hivi sasa hawanunui kwetu na wanatueleza kuwa wananunua mayai hayo kwa wafanyabiashara kutoka Kenya,” Aliongeza, “Wanatueleza wazi kuwa mayai hayo yanauzika kwa wafanyabiashara wa vyakula kwa kuwa si rahisi kuonekana na watumiaji kama yana kasoro, ila kwa watu ambao hununua mayai kwa ajili ya kuwauzia watu wengine, huyakataa mayai hayo kwa sababu hayauziki na baadhi ya watu wameanza kuyagundua hayafai.”

Alisisitiza kuwa uingizwaji wa mayai hayo nchini unawapa wakati mgumu kwa kuwa wengi wao wamechukua mikopo katika benki mbalimbali nchini, hivyo kitendo cha kuuza trei moja kwa Sh 5000 kinawafanya wapate hasara. Mmoja wa wafanyabiasha hao, Mseti Marwa alisema; “Kama serikali imeruhusu mayai haya yaingie nchini basi wote tuuze bei moja, pia kama wafanyabiashara hawa wana kibali cha kuuza bidhaa hii basi serikali inatakiwa kushusha viwango vya bei za vyakula vya kuku na dawa ili tuweze kuuza kwa bei inayofanana”.

Katika hatua nyingine wafanyabishara hao walilalamikia kampuni za kuuza vifaranga nchini kutokana na vifaranga hivyo kutokuwa na ubora unaotakiwa. “Unaweza kukuta unanunua vifaranga 500 lakini vinatoa mayai trei nane hadi saba tu kitu ambacho si cha kawaida…, katika malalamiko yetu tutaitaka serikali ituruhusu tununue vifaranga kutoka nje ya nchi,” alisema Bambanza Kauli ya serikali Akizungumzia suala hilo Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo alisema kuwa yuko tayari kuyapokea malalamiko ya wafanyabiashara hao na kuyafanyia kazi.

“Hilo jambo ndio kwanza nalisikia kutoka kwao… Ila serikali ipo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa soko la ndani linaimarika hivyo nawasubiri ili nisikilize malalamiko yao na nitayafanyia kazi,” alisema Dk Mathayo. Akizungumzia suala la wafanyabiashara kununua vifaranga nje ya nchi alisema, “Wanaweza kufanya hivyo ila ni mpaka wapate vibal.”

Hospitali ya Mount Meru yadaiwa kuua mjamzito

HOSPITALI ya Mkoa wa Arusha Mount Meru imeingia kwenye kashfa baada ya baadhi ya madaktari wake na wauguzi kutuhumiwa kusababisha kifo cha mjamzito ,Florence Joseph (34) mkazi wa Sokoni one jijini Arusha.

Mwili wa marehemu huyo pamoja na kichanga chake tayari imezikwa juzi katika makaburi ya Njiro yaliyopo nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Mganga mkuu wa hospitali hiyo,Dk Omar Chande alipohojiwa kuhusu tukio hilo alisema kwamba bado hajapokea taarifa hiyo, lakini aliahidi kufuatilia kwa kina kabla ya kutoa ufafanuzi wa kina.


Akisimulia kisa hicho jirani wa wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Katrina Kimaro katika eneo la msiba huo alisema kwamba Febuari 19, mwaka huu saa 10.00 jioni alimsindikiza marehemu kujifungua katika Hospitali ya Levolosi iliyopo jijini hapa baada ya kushikwa na uchungu mkali.

Alisema kwamba mara baada ya kufika hospitalini hapo madaktari katika hospitali hiyo walimpima na kisha kushauri apelekwe haraka Hospitali ya Mount Meru kutokana na kuona njia ya kujifungua ikiwa ndogo.

Katrina, alisema kwamba walifika katika hospitali hiyo saa 12.00 jioni ambapo moja kwa moja waliwasili eneo la mapokezi na kuambiwa wasubiri watahudumiwa lakini cha ajabu kila daktari aliyekuwa akipita eneo hilo alikuwa akiwashangaa.

Alisema kwamba wakati wanaendelea kusubiri katika eneo la mapokezi hospitalini hapo marehemu alikuwa akilalamika mara kwa mara kwamba anasikia uchungu mkali ndipo alipowafuata wauguzi waliokuwapo katika chumba cha mapokezi lakini walimjibu wana shughuli nyingi zinazowaingizia pesa.

“Tulipokuwa eneo la mapokezi marehemu alikuwa akijisikia uchungu mkali kila mara analalamika ikabidi mimi niwafuate wauguzi niwaeleze lakini cha ajabu walinijibu kwamba wana kazi zingine, wanakula vichwa” alisema Kimaro.

Aliendelea kusimulia kisa hicho kwamba ilipofika saa 2.00 usiku alijitokeza daktari mmojawapo aliyewauliza shida yao na ndipo walipomweleza ambapo alifanya taratibu za marehemu kufikishwa katika chumba cha kuzalia na wao waliambiwa warudi nyumbani marehemu atahudumiwa.

Alisema kwamba kesho yake Febuari 20, alfajiri saa 11.00 alifika hospitalini hapo kujua hali ya marehemu endapo ameshajifungua au la na ndipo alipoenda moja kwa moja katika wodi ya wazazi hospitalini hapo na kumtafuta bila mafanikio.

Alisema baada ya hali hiyo ndipo alipokwenda katika ofisi za chumba cha kuzalia na kumkuta muuguzi mmojawapo na kumwulizia marehemu, lakini cha ajabu muuguzi huyo alitokomea bila kumpa jibu lolote na ndipo alipoamua kwenda katika lango kuu la hospitali hiyo kumwuliza askari aliyekuwa akilinda langoni hapo.

Kimaro, alibainisha kwamba askari huyo alimchukua na kisha kumfikisha kwa muuguzi mwingine waliyemkuta katika wodi ya wazazi akifanya usafi ambapo baada ya kumwelezea shida yake cha ajabu aliwajibu kwamba ametingwa na hawezi kuacha kufanya usafi ashughulikie suala lao.

Alidai baada ya hali hiyo ndipo alipojitokeza daktari mmojawapo baada ya kumwona akihangaika na alipomweleza shida yake akampeleka kwa muuguzi mmojawapo ambaye yuko katika ofisi za chumba cha kuzalia na alipomweleza shida yake alimjibu kwamba wanasikitika mgonjwa wake alifariki jana katika mazingira ya kutatanisha.

Kimaro alisema kwamba muuguzi huyo alimpa maelezo kwamba ilipofika saa 6.00 usiku jopo la madaktari walienda kumchunguza marehemu endapo njia ya kujifungulia imefunguka na ndipo walipompa muda saa moja na kisha kurudi tena saa 7.00 usiku ambapo walimchukua kwa lengo la kwenda kumfanyia upasuaji lakini tayari alikuwa ameshafariki dunia.

“Nakumbuka yule muuguzi alinieleza kwamba ilipofika saa sita usiku walishuka katika chumba cha kuzalia lakini wakamkuta marehemu ana uchungu mkali na njia haijafunguka ndipo walipompa saa moja tena wakarudi saa saba na kuamua kumchukua kumpeleka kumfanyia upasuaji lakini tayari walimkuta marehemu alikuwa ameshakata roho”alisema kwa uchungu

Naye, mume wa marehemu huyo ,Rashid Aloyce alilalamikia kifo cha marehemu mke wake na mtoto kwamba kimetokana na uzembe wa madaktari hospitalini hapo kwa kuwa walimwacha kwa muda wa saa saba bila kumpatia huduma yoyote pamoja na kushikwa uchungu mkali.

Giggs mkongwe aliyecheza mechi 900 Man. United

LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amempongeza mkongwe wake, Ryan Giggs akisema ni kati ya wachezaji wanaozeeka huku kiwango cha soka kikiwa bado juu.

Giggs, 38, ambaye amecheza mechi 900 za United kaika mashindano yote, ni kati ya wachezaji wanaotarajiwa kupewa heshima katika klabu hiyo kwa utumishi wa muda mrefu.

Hiyo itamfanya Giggs kuendelea kuuwania ubingwa ikiwa ni pamoja na kuwa miongoni mwa wachezaji wa pambano la Norwich lililopigwa jana na Ferguson anaamini kuwa hakuna mchezaji kama yeye.

"Kwa mtazamo wangu, na siamini kama kila mmoja atakubaliana na mimi, kuwemo kwenye Ligi Kuu na licha ya kufaya makubwa, siamini kama kuna mchezaji mwingine anaweza kumfikia," anasema kocha wa United juzi.

"Pamoja na ukongwe wake, anajaribu kutengeneza mazingira mazuri kufanikisha azma ya uchezaji wake. Anacheza kiwango cha juu, na leo, anacheza kama wachezaji wengine. Anafurahisha."

Ferguson anaamini kuwa kujituma, kujitunza na kufuata taratibu za mchezo ndicho kilichomfanya Giggs kucheza kwa muda mrefu.

"Giggs ni kati ya wachezaji waliokomaa, amekuwa akikimbiza vizuri na zaidi hupenda kusimama namba za katikati ya dimba la mbele. Huopewa nafasi kama mchezaji wa kipekee kwenye timu," anasema.

"Itakumbukwa Ryan a mekuwa mchezaji mashuhuri kwa kupanda na kushuka na mch ezaji makini sana anapokuwa uwanjani.

"Amekuwa akibadilika sana na amekuwa akibadilika tofauti na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita na anapokuwa mchezoni anaonekana tofauti na unavyomdhania."

Giggs ameingia mkataba wa mwaka mmoja, utakaomfanya abaki Old Trafford hadi mwisho wa msimu wa 2013 na, pia amecheza mechi 64 na timu ya taifa ya Wales na mbili za U-21 na lengo lake ni kufikisha mechi 1,000 kabla ya kustaafu soka.

"Juu ya umri," Ferguson, anasema kuwa hilo linawezekana.

"Stanley Matthews amecheza soka akiwa na miaka 50, tusubiri kwa Giggs na tuone."

*Maisha ya Giggs
Ryan Joseph Wilson ni mtoto wa kufikia aliyelelewa katika kituo cha St David's Hospital mjini Canton, Cardiff, cha Danny Wilson,

Akiwa na umri mdogo Giggs amekulia katika eneo la Ely, magharibi mwa Cardiff. Mdogo wake, Rhodri, alikuwa akiichezea klabu ya Salford City.

Ametumia muda mwingi kucheza barabarani na watoto wenzake kwenye mji wa Pentrebane. Mwaka 1980, Giggs akiwa na miaka sita, alisaini Swinton RLFC, na familia nzima ikahamia Swinton, katika mji wa Salford, Greater Manchester.

Mwaka 1990-1995, alianza kuichezea Manchesster United kwani alipewa mkataba Novemba 29, 1990 (akiwa na miaka 17). Alianza kucheza soka kama mwanasoka wa kulipwa (1 Desemba 1990).

Akiwa na timu hiyo kombe lake la kwanza lilikuwa FA na kimsingi Giggs alianza kuichezea timu yake dhidi ya Everton kwenye Uwanja wa Old Trafford Machi 2, 1991 akitokea benchi kuchukua nafasi ya Denis Irwin.

Giggs alianza kuichezea timu ya kwanza akiwa na miaka 17, na kuweka rekodi yake kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuitumikia Manchester United. Huo ukawa mwanzo wa kuitumikia klabu ya wakubwa ya Ferguson

Arsenal yaingia mwaka wa saba bila ubingwa

LONDON, England
WIKI mbili zilizopita, zilikuwa mbaya kwa mashabiki wa Arsenal. Katika kipindi cha siku nne, the Gunners ilichapwa na AC Milan 4-0, na kuififisha nafasi ya Arsenal kuendelea na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na Jumamosi Februari, 18, Sunderland iliwaliza Gunners 2-0.

Kwa hali hiyo, inafanya kikosi cha Arsene Wenger kumaliza msimu wa saba bila ubingwa na zaidi ni baada ya kufungwa mechi ya Sunderland.

Arsenal inatakiwa kufanya mabadiliko makubwa na zaidi katika kutengeneza kikosi cha kwanza kwanza. Kwa mujibu wa Sunday Mirror, miongoni mwa watu wa ngazi za juu wa Gunners kuna haja ya kufanyia mabadiliko safu nzima ya timu.

Manchester City imeanza kuiga staili ya Arsenal kwani imeanza kutengeneza wachezaji chipukizi. Cha kushangaza, Wenger na uongozi mzima wa Arsenal wanashindwa kutoka kupitia mazao ya chipukizi wao.

Mpango wa sasa ni kumpatia Wenger uwezo wa kusajili wachezaji wakubwa na kuongeza mishahara kwa wachezaji waliopo, Robin van Persie, Arsenal ni miongoni mwa wachezaji watakaoneemeka.

Robin van Persie amebakisha mwaka mmoja kumaliza mkataba wake na Arsenal. Bosi ya klabu kwa sasa inazungumza na Wenger kwa ajili ya kununua wachezaji wakubwa kuibeba klabu.

Baadhi wameanza kusema kuwa hali ni mbaya kwa sasa Arsenal katika historia ya uongozi wake na kwamba mechi mbili zilizopita, zimekuwa tatizo.

Ni wakati kwa Arsenal kufanya maamuzi magumu. Inatakiwa kutengeneza timu kutoka uwanjani hadi kwa wachezaji mmoja mmoja kwani vinginevyo mashabiki wanaweza wasinunue ama kubakia vyooni wakiangalia kupitia kwenye televisheni.

Chelsea yachanja...

LONDON, England
CHELSEA imeendelea kuchanja mbuga baada ya kuibandua Bolton mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya England na kumaliza ukame wa ushindi wa timu hiyo wa mechi tano mfululizo.

Bolton iliyokuwa imeikaba Blues lakini kabla ya mapumziko, Mbrazil, David Luiz alitupia mpira ndani ya kimia kuandika bao la kwanza kwa timu yake.

Didier Drogba alipiga kichwa cha karibu na kufanya matokeo kuwa 2-0 kabla ya Frank Lampard kumalizia krosi ya Juan Mata.

Wageni walipoteza nafasi baada ya Ryo Miyaichi kukosa bao la wazi ambalo lingewafanya kuwa mbele kabla ya Chelsea kufunga. Chelsea imefikisha pointi 46 na kuishusha Arsenal ambayo jana ilikuwa na kazi dhidi ya Tottenham.

Mechi nyingine za jana usiku, Norwich ilikuwa ikicheza na Man United huku Stoke ikiikaribisha Swansea.

Mbali na mechi hizo, West Brom iliyokuwa nyumbani hiyo juzi, iliitandika Sunderland mabao 4-0. Sunderland iliifunga Arsenal katika moja ya mechi za ligi hiyo hivi karibuni.

Nayo QPR ilishindwa kutumia uwanja wa nyumbani na kuchapwa bao 1-0 na Fulham wakati Newcastle ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya 2-2 na Wolves. Wigan na Aston Villa zenyewe zilitoka suluhu katika mfululizo wa mechi hizo.

Watanzania wachemka Kili Marathon


Wanariadha wa Kenya, Ezekiel Kimath (kushoto) Kimot Chemo na David Kipromo, wakiongoza mbio za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika mjini Moshi jana. Wanariadha hao walitamba kwa kuchukua nafasi zote 20 za juu kwa upande wa wanaume na wanawake. Picha na Mussa Zumba.

TANZANIA imeendelea kuwa msindikizaji katika medani ya kimataifa baada ya wanariadha wake pekee, Fabian Joseph kushika nafasi ya tatu kwa upande wa wanaume na Mary Naali kushika nafasi ya tano kwa upande wa wanawake katika mbio za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Wakati hali ikiwa mbaya kwa wanariadha wa Tanzania, Kenya imeendelea kutawala mbio hizo baada ya wanariadha wake (wanaume kwa wanawake) kukamata nafasi zote tatu muhimu za juu katika mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Premium Lager na Nusu Marathon Kilometa 21.

Katika mbio hizo, Joseph alikamata nafasi ya tatu katika mbio za nusu marathon kwa upande wa wanaume baada ya kutumia saa 1:03:32 na kuzawadiwa medali ya shaba wakati Naali alikamata nafasi ya tano katika mbio za nusu marathon baada ya kutumia saa 1:15:47 kwa upande wa wanawake.

Umahiri wa Wakenya ulianzia katika mbio za Kilimanjaro Marathon za Kilometa 42 kwa upande wa wanaume, ambapo David Kipron aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 2:13:57, wakati Ezekil Kimtai alikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 2:14:06 huku Kibeth Timoth akimaliza mshindi wa tatu kwa kutumia saa 2:15:38.

Uhodari huo wa Wakenya hao uliendelea kwa upande wa wanawake ambapo Monica Jopkoech alimaliza mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 2:42:45 wakati Peris Jepkorir alishika nafasi ya pili baada ya kutumia saa 2:43:02 na Panuelag Anesomi alitwaa nafasi ya tatu akitumia saa 2:43:41.

Katika mbio za nusu marathon, Hosea Mallel aliendeleza wimbi la ushindi kwa Wakenya alipotumia saa 1:03:00 na kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume, wakati Ngengi Jofrey alikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 1:03:32 na kumwacha Mtanzania Joseph akikamata nafasi ya tatu alipotumia saa 1:03:14.

Naye Vicoty Chepkemoi alikuwa mbabe kwa upande wa wanawake alipoibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia saa 1:13:00, huku Wakenya wenzake Cythia Limo akikamata nafasi ya pili baada ya kutumia saa 1:13:07 na Flomena Daniel aliyemaliza akiwa katika nafasi ya tatu baada ya kutumia saa 1:14:48.

Kivumbi kingine kilikuwa katika mbio za kujifurahisha, ambapo Gareth Ismail aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume wakati Brazil Boy alishika nafasi ya pili na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Fabia Nelson wakati ambapo Jaquline Juma aliibuka mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanawake, akimwacha Catherine Yuko katika nafasi ya pili na Nathaniel Elisante aliyemaliza katika nafasi ya tatu.

Washindi wa kwanza wa mbio za Kilimanjaro Marathon (wanawake na wanaume) walizawadiwa Sh 6 milioni, Sh 3 kwa washindi wa pili na 1,500,000 kwa washindi wa tatu,huku zawadi hizo zikiendelea katika mtitiriko wake.

Naye mshindi wa pili wa mbio za nusu marathon (wanaume kwa wanawake) walizawadiwa Sh 3 milioni, mshindi wa pili Sh 1,500,000 na mshindi wa tatu Sh 750,000 kwa mtiririko wake huku washindi wa mbio nyingine kama za kujifurahisha na Gapco pia walipata zawadi mbalimbali ikiwamo fedha taslimu.